Jeshi la polisi nchini Tanzania limetoa ufafanuzi kuwa halijazuia mikutano ya vyama vya kisiasa
Katika taarifa yake,limesema kuwa kile lilichozuia ni mikutano ya hadhara ambayo lilihisi itavuruga hali ya usalama
Hivyobasi jeshi hilo sasa limewataka wananchi kupuuza taarifa kuwa wao walizuia mikutano ya kisiasa.
"Jeshi la Polisi linapiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia tarehe 07/06/2016 hadi hapo hali ya kiusalama itakapotengemaa."
Kulingana na nukuu hiyo jeshi hilo linasema kuwa hakuna sehemu yoyote iliyopiga marufuku mikutano ya kiutendaji na kiutawala ya vyama vya kisiasa inayofanywa kwa mujibu wa katiba na kanuni za vyama husika.
Jeshi hilo limetoa mfano wa Chama cha CUF kilichotangaza kuwa kimepanga kufanya mkutano mkuu kujaza nafasi ya Mwenyekiti wao wa Taifa tarehe 21 Agosti, 2016,na ambao Polisi hawakujitokeza kuuzuia.
Taarifa kutoka Sudan Kusini zinasema mamia ya watu, wengi wao wakiwa ni wanajeshi wameuawa katika mapambano baina ya vikosi vyenye uhasama katika mji mkuu wa Juba.
Mwandishi mmoja wa habari aliyeko mjini Juba amesema mapigano yameendelea mpaka mapema saa za asubuh ya Jumamosi.
Wanajeshi wametanda kwenye mitaa huku watu wachache wakionekana kutoka nje.
Daktari mmoja amesema mili mingi imepelekwa hospitali huku chumba cha kuhifadhia maiti kikiwa kimejaa.
Mapigano baina ya wanajeshi watiifu wa Rais Salva Kiiri dhidi ya Makamu wa rais Riek Machar yalianza tangu siku ya Alhamis.
Sudan Kusini inatimiza miaka mitano ya Uhuru na kuanzishwa kwake lakini hakuna sherehe zitakazofanywa.
Marekani na Korea Kusini zimekubaliana kuweka mfumo wenye utata wa ulinzi dhidi ya makombora, kama njia ya kukakabiliana na vitisho vinayoendelea kutoka kwa Korea kaskazini.
Mfumo huo wa ulinzi unaowekwa katika maeneo yenye milima mirefu kudhibiti mashambulizi ya makombora utawekwa kujibu vitisho tisho kutoka Pyongyang, ilieleza taarifa.
Haijabainika wazi ni wapi mtambo huo utawekwa na hatimae ni nani ataudhibiti.
Uchina, ambayo imekuwa ikipinga mara kwa mara mpango huo, imepinga mfumo huo tena kupitia wajumbe wa korea Kusini na Marekani.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uchina amesema kuwa mfumo wa THAAD utadhuru amani na utulivu katika kanda hiyo, licha ya uwezo wake wa kugundua na kulipua makombora ya Korea Kaskazini.
"Uchina inaelezea kutoridhishwa kwake na kupinga vikali hili'', ilisema katika taarifa kupitia mtandao wake.
Maafisa watano wa polisi mjini Dallas, Marekani wamepigwa risasi na kuuawa wakati wa maandamano ya kupinga mauaji ya watu weusi.
Maafisa wengine sita wanauguza majeraha.
Maafisa wa polisi katika mji ulio katika jimbo la Texas, wanasema mauaji hayo yametekelezwa na washambuliaji wawili wa kulenga shabaha.
Mkuu wa polisi wa Dallas David Brown amesema amesema maafisa wa polisi bado wanakabiliana na mshukiwa mmoja ambaye anadaiwa kujibanza katika jumba linalotumiwa kuegesha magari.
“Mshukiwa huyo ambaye tunawasiliana naye amewaambia maafisa wetu kwamba mwisho unakaribia na kwamba ataumiza na kuua wenzetu wengi, akimaanisha maafisa wa usalama na kwamba kuna mabomu yaliyotegwa eneo lote, kwenye gereji na katikati mwa jiji.”
Vyombo vya habari jimbo hilo vinasema kumetokea mlipuko mkubwa eneo hilo lakini habari hizo hazijathibitishwa.
Bw Brown amesema mwanamke aliyekuwa karibu na eneo alimojificha mwanamume huyo anahojiwa na maafisa wa usalama.
“Hatuwezi kusema kwamba tumewakamata washukiwa wote,” alisema mkuu huyo wa polisi.
Ufyatuaji risasi ulitokea mwendo wa saa tatu kasorobo usiku saa za Texas waandamanaji walipokuwa wakipitia barabara za mji na kuwafanya waandamanaji kukimbilia usalama wao.
Maandamano hayo yalitokana na kuuawa kwa wanaume wawili weusi, Philando Castile jimbo la Minnesota na Alton Sterling eneo la Baton Rouge jimbo la Louisiana.
Miongoni mwa maafisa wa polisi waliofariki ni afisa wa trafiki Brent Thompson, 43.
Raia mmoja, ambaye jamaa zake wamesema jina lake ni Shetamia Taylor, alipigwa risasi mguuni akiwakinga watoto wake na kwa sasa anapokea matibabu hospitalini.
Meya wa Dallas Mike Rawlings amesema "huu ni wakati wa kusikitisha sana kwa jiji letu.”
Rais wa Marekani Barack Obama, akirejelea takwimu zinazoonesha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa Wamarekani Weusi kupigwa risasi na maafisa wa polisi kuliko Wamarekani Wazungu, amesema ubaguzi huo unafaa kumalizwa.
"Visa kama hivi vinapotokea, kuna sehemu kubwa ya raia wanaohisi kwamba kwa hawatendewi haki kwa sababu ya rangi ya ngozi zao, kwa sababu hawatazamwi kwa njia sawa. Na hili linauma,” amesema.
Takwimu kutoka kwa shirika linalotetea maafisa wa polisi Marekani la Officer Down Memorial zinaonesha maafisa 53 wa polisi wameuawa wakiwa kazini mwaka 2016, 21 wakiuawa kwa kupigwa risasi. Idadi hiyo haijumuishi maafisa waliouawa Dallas.
Watu 12 wamefariki nchini Indonesia kutokana na foleni ya magari iliyosababisha mamilioni ya watu kukwama barabarani siku kadha.
Wengi walifariki kutokana na kukosa maji mwilini na uchovu.
Watu wengi waliokuwa wakisafiri kwa sherehe za kuadhimisha mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhan walikusanyika katika makutano ya barabara kisiwa cha Java.
Na hapo ndipo msongamano mkubwa wa magari ulipotokea.
Mamia ya watu watavua nguo zao na kupigwa picha wakiwa tupu kusherehekea utamaduni katika mji wa Hull, Uingereza.
Tukio hilo litakuwa la kusherehekea mji huo kama Mji wa Utamaduni.
Washiriki watapakwa rangi ya samawati Jumamosi na kisha wapigwe picha wakiwa katika maeneo mashuhuri jijini humo kama sehemu ya mradi uliopewa jina Sea of Hull.
Mradi huo unatekelezwa na mpiga picha Spencer Tunick na unadhaminiwa na taasisi ya Sanaa ya Ferens Art Gallery.
Picha zitakazopigwa zitawekwa na kuoneshwa kwa umma wakati wa tamasha ya sanaa ya 2017 itakayoendelea kwa mwaka mmoja.
Tunick, anayetoka New York, amewahi kufanya kazi kama hiyo kwingine.
Amewahi kupiga picha za watu wengi wakiwa uchi Sydney Opera House, Place des Arts mjini Montreal, Mexico City na mjini Munich nchini Ujerumani Germany.
Bw Tunick amesema kazi zake “hugusia historia ndefu ya Sanaa ya utupu”.
"Mavazi ni Sanaa ya mtu mwingine,” anasema.
“Fashoni ni Sanaa. Kwa kuondoa hilo (mavazi), nitakuwa nafanya kazi na usawa na maumbile katika umaridadi wake.”
Watu karibu 2,000 wamejiandikisha kupigwa picha tangu wazo hilo litangazwe mwezi Machi.
Baraza la mji wa Hull limesema baadhi ya barabara zitafungwa wakati wa shughuli hiyo Jumamosi asubuhi.
Madaktari nchini India wamepandikiza pua mpya katika uso wa mvulana wa miaka 12 iliokuwa imemea katika paa lake la uso.
Pua ya Arun Patel iliharibika alipougua ugonjwa wa homa ya kichomi
Maambukizi hayo yaliharibu pua yake akiwa mtoto mdogo.
Upandikizaji kama huo ulifanywa nchini China mwaka 2013 ambapo mtu mmoja ambaye aliharibu pua yake katika ajali alipewa pua mpya.
Wazazi wa Arun walimchukua na kumpeleka katika daktari mwengine katika kijiji cha jimbo la kati la Madhya Pradesh ambapo aliugua kichomi mda mfupi baada ya kuzaliwa.
Lakini matibabu aliyopewa yaliongeza hali yake na hivyobasi kupoteza pua yake.
Miaka kadhaa baadaye,kundi moja la madaktari katika mji wa Indore liliamua kufanya upasuaji usiokuwa wa kawaida ambapo Arun alipata pua mpya.
Mchezaji nyota wa Argentina na Barcelona Lionel Messi amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela baada ya kupatikana na makosa ya kutumia ulaghai wakati wa ulipaji ushuru, vyombo vya habari nchini Uhispania vinaripoti.
Babake, Jorge Messi, pia amehukumiwa kufungwa jela kwa kuilaghai Uhispania €4.1m (£3.2m; $4.6m) kati ya 2007 na 2009.
Wakati wa kesi, waendesha mashtaka walisema maeneo salama yenye kinga dhidi ya ushuru Belize na Uruguay yaliyumiwa kuficha mapato kutokana na uuzaji wa haki za picha za mchezaji huyo.
Lakini Messi amesema hakufahamu lolote kuhusu masuala yake ya kifedha.
Wawili hao hata hivyo hawatarajiwi kufungwa jela.
Chini ya mfumo wa haki nchini Uhispania, mtu anaweza kutumikia kifungo chochote kilicho chini ya miaka miwili nje ya gereza.
Messi na babake pia wanaweza kukata rufaa katika Mahakama ya Juu nchini humo.