Jumatatu, 4 Julai 2016

Mamia waandamana kupinga mauaji Kenya



Mashirika
Image captionMashirika ya kutetea haki za kibinadamu wanataka waliohusika waadhibiwe
Mamia ya watu wameandamana jijini Nairobi, Kenya kupinga mauaji ya kiholela ambayo yanadaiwa kutekelezwa na maafisa wa usalama nchini humo.
Maandamano hayo yamefanyika kufuatia kupatikana kwa miili ya wakili Willie Kimani, mteja wake Josephat Mwendwa na dereva wa teksi Joseph Muiruri.
Bw Kimani na Bw Mwenda walikuwa wameabiri gari la Bw Muiruri baada ya kuhudhuria kesi katika mahakama ya Mavoko 23 Juni, walipotekwa na watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa usalama.
Inadaiwa walizuiliwa kwa muda katika kituo cha polisi wa utawala cha Syokimau.
Miili yao ilipatikana katika mto wa Ol Donyo Sabuk, jimbo la Machakos, mashariki mwa jiji la Nairobi, ikiwa imefungwa mkono na ikionekana kuwa na ishara za majeraha.
"Mauaji ya vijana hawa watatu yanafaa kumtia wasiwasi Rais Kenyatta," amesema Bw George Kegoro, mkurugenzi mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Tume ya Haki za Binadamu Kenya.
"Kiongozi wa nchi ni sharti aunde jopo la uchunguzi kuhusu kutekwa na kutumiwa vibayakwa idara za polisi na rasilimali zake kwa manufaa ya watu binafsi na katika kutekeleza uhalifu ikiwa ni pamoja na, katika kisa hiki, mauaji ya kiholela."

Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) kimewashauri wanachama wake kususia shughuli za mahakama kulalamikia kuuawa kwa wakili mwenzao, Bw Kimani.
Waandamanaji wameanzia msafara wao eneo la Freedom Corner, uwanja wa Uhuru Park na kupitia katikati mwa jiji ambapo watafika pia makao makuu ya polisi na makao makuu ya idara ya mahakama.
Baadhi ya mashirika ya kutetea haki za kibinadamu wanataka Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet na Waziri wa Usalama Joseph Nkaissery wajiuzulu.
Kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali linalofuatilia visa vya ukatili wa polisi dhidi ya raia Kenya la IMLU, mwaka 2015 watu 125 waliuawa kiholela na maafisa wa polisi.
Maandamano
Image captionWaandamanaji nje ya Mahakama ya Juu, Nairobi
Kati ya Januari na Aprili mwaka huu, watu 53 tayari wameuawa kwa mujibu wa IMLU.
Maafisa watatu wa polisi waliotuhumiwa kuhusika katika kutoweka kwa Bw Kimani, Bw Mwenda na Bw Muiruri wamekuwa wakizuiliwa na walitarajiwa kufikishwa kortini leo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

SOMA ZAIDI HAPA