Jumatatu, 11 Julai 2016

Uganda yatuma wanajeshi mpaka wa Sudan Kusini




Image copyrightREUTERS
Image captionNdege zatumika katika mapigano Sudan Kusini
Uganda imetangaza kwamba itatuma wanajeshi wake katika mpaka wake na Sudan Kusini baada ya mapigano kuzuka upya nchini humo.
Msemaji wa jeshi la Uganda Paddy Ankunda amesema wanajeshi hao watatumwa kuzuia mapigano kuenea hadi maeneo ya Uganda.
Wakati huo huo baraza la usalama la Umoja wa mataifa, linawaomba viongozi wakuu wa serikali ya Sudan Kusini, kuyadhibiti majeshi yao.
UN inasema kuwa mashambulio dhidi ya raia na makao makuu pamoja na kambi ya Jeshi ya Umoja wa mataifa, ni uhalifu wa kivita.
Walinda amani wawili wa umoja wa mataifa kutoka Uchina, wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Umoja wa mataifa unasema kwamba, mataifa jirani na Uchina yanafaa kujiandaa kutuma majeshi zaidi nchini humo, ikiwa hali ya usalama itaendelea kudorora .
Image copyrightREUTERS
Image captionWanajeshi wakishika doria mabarabarani katika mji mkuu wa Juba
Hata hivyo baraza hilo litahitaji kuidhinisha vikosi zaidi.
Kwa sasa wanajeshi wa umoja wa mataifa walioko Juba ni elfu 13 pekee.
Umoja wa mataifa unasema kuwa, walinda amani wanafaa kutumia kila mbinu kuwalinda raia.
Waandishi wa habari wameiambia BBC kuwa ndege za helikopta zimetumika kurusha risasi pande zote huku zikishambulia majengo ya maskani ya bwana Machar.
Image copyrightAFP
Image captionWanajeshi watiifu kwa rais Salva Kiir na wale watiifu kwa Riek Machar wamekuwa wakipigana tangu Alhamisi
Milio mikubwa ya risasi ilisikika katika makao makuu ya kambi ya kijeshi ya umoja wa mataifa.
Vifaru vya kivita vinaonekana katika barabara za mji mkuu Juba, huku wakaazi wakijifungia ndani ya majumba yao.
Mamia ya watu wameuwawa tangu ghasia hizo zianze upya siku tano zilizopita.
Mapigano yaliyoripotiwa kutokea katika uwanja wa ndege mjini Juba, yamesitishwa, huku mashirika mbalimbali ya usafiri wa ndege kuingia na kutoka mjini Juba, likiwemo shirika la ndege nchini Kenya -KQ yamesitisha usafiri.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

SOMA ZAIDI HAPA